Chama cha Hakimiliki ya Muziki Nchini Kenya – MCSK kimesema kwamba kamwe hakitavumilia hujuma ya aina yoyote ya kiuchumi dhidi ya wanachama wake.
Katika taarifa mkurugenzi mtendaji wa MCSK Ezekiel Mutua alilaani vikali wito wa viongozi wa kisiasa wa hivi majuzi wa kususia muziki wa baadhi ya wasanii wa Kenya, akitaja hatua hiyo kuwa uhujumu wa kiuchumi unaotishia riziki za wanachama wake.
Mutua, alikosoa miito hiyo ya kususia, iliyozuka baada ya kundi la wasanii kutoka eneo la Mlima Kenya kukutana na Naibu Rais Kithure Kindiki wikendi iliyopita.
Chama hicho kilieleza kuwa wasanii hao walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya uhuru wa kushirikiana.
“Tunasikitishwa sana na miito ya viongozi wakuu wa kisiasa ya kususia kazi za wanachama wetu,” alisema Mutua akiongeza kwamba ni muhimu kufahamu wazi kwamba, “MCSK haitavumilia aina yoyote ya hujuma ya kiuchumi inayolenga wanachama wetu”.
MCSK ilionya kwamba kumbi za burudani zitakazobainika kubagua wasanii kwa kutekeleza wito huo wa kususia hazitaruhusiwa kupiga muziki uliyoidhinishwa na chama hicho.
“Maonyesho ya hadhara ni chanzo kikuu cha mapato kwa wasanii wetu,” ilisema taarifa ya Mutua na kuendelea kwamba “Kuanzisha hatua za kisiasa zenye mgawanyiko zinazotishia riziki ni sawa na kubomoa misingi ya kazi yao ya ubunifu”.
Chama hicho pia kilitoa wito wa mshikamano miongoni mwa wasanii na kuwasihi wadau katika sekta ya burudani kupinga shinikizo za kuingiza siasa katika tasnia ya muziki.
Dkt. Mutua alisisitiza jukumu muhimu wanalotekeleza wasanii katika kukuza umoja, uponyaji na mshikamano wa kitaifa hasa nyakati za migawanyiko ya kikabila.
“Muziki ni lugha ya ulimwengu inayowaunganisha watu bila mipaka. Hali za kisiasa za muda hazipaswi kuruhusiwa kupunguza maana hii pana ya muziki” alisema.
MCSK ilisisitiza tena kujitolea kwake kulinda wanachama wake dhidi ya ubaguzi na ikaahidi kufuatilia hali hiyo kwa karibu huku ikichukua hatua stahiki kulinda sekta ya ubunifu.