Kenya na Morocco siku ya Jumatatu, zilitia saini Mikataba ya Maelewano kwa lengo la kuboresha uhusiano na kupanua ushirikiano katika sekta muhimu kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini mikataba hiyo Jijini Rabat, Morocco ambako ujumbe wa Kenya ulikuwa mgeni wa waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Nasser Bourita, waziri wa Mambo ya Nje na Maswala ya Ughaibuni Musalia Mudavadi, alielezea kujitolea kwa serikali ya Kenya kuhakikisha mikataba hiyo inanufaisha mataifa hayo mawili.
“Wakati wa ziara hiyo, Kenya na Morocco zilitia saini Mikataba ya Ushirikiano katika sekta za Maendeleo na Nyumba, Biashara, Maswala ya Vijana yale ya Kimataifa na kati ya Tasisi ya Serikali na ile ya Elimu ya Juu na Usimamizi ya Morocco,” alisema Mudavadi.
Katika ziara hiyo nchini Morocco, Mudavadi alisema alipigia debe uuzaji wa Chai na Kahawa ya Kenya nchini humo ili kuhakikisha usawa wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Aidha alisema alipendekeza kuongezwa kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa hapa nchini nchini Morocco, pamoja na kuajiriwa kwa walimu wa Kenya nchini humo kukidhi hitaji la walimu wa Kiingereza linaloshuhudiwa katika taifa hilo la Kiarabu.
Ziara hiyo ni hatua kubwa katika kupiga jeki ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kuimaridsha maendeleo ya pamoja.