Msigwa ampigia debe Abi Chams

Abi Chams aliandikisha historia ya kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kuwahi kuteuliwa kuwania tuzo za BET.

Marion Bosire
1 Min Read

Katibu mkuu wa wizara ya habari utamaduni,sanaa na michezo nchini Tanzania Gerson Msigwa ambaye pia ni msemaji mkuu wa serikali amempigia debe mwanamuziki Abi Chams.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Msigwa alichapisha video inayomwonyesha akiomba raia wa tanzania waunge mkono binti yao Chams ambaye anawania tuzo ya BET.

Msemaji huyo wa serikali aliwaelekeza kabisa watu wa Tanzania kuhusu namna ya kupiga kura hizo ikiwa imesalia siku moja pekee kabla ya shughuli ya kupiga kura kufungwa.

Abi Chams anawania tuzo katika kitengo cha mwanamuziki mpya bora kimataifa yaani Best International Act, na ndiye msanii wa kwanza wa kike kuwahi kuteuliwa kuwania tuzo hizo za BET.

Msanii huyo ameungwa mkono na wasanii kadhaa nchini Tanzania ambao pia wamekuwa wakimpigia debe akiwemo Harmonize, Young Lunya, Barnaba Classic, Rayvanny na Vanessa Mdee.

Hafla ya kugawa tuzo za BET itaandaliwa Jumatatu Juni 9, 2025 katika ukumbi wa Peacock ulioko Los Angeles, California nchini Marekani.

Share This Article