Akothee atangaza kwamba anahamia Ufaransa

Ameafikia uamuzi huu kufuatia kile anachokitaja kuwa maamuzi ya wanawe.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya ambaye pia ni mhisani Akothee ametangaza mipango ya kuhamia Ufaransa, hatua ya mabadiliko makubwa katika maisha yake.

Akothee ambaye pia hujirejelea kama Rais wa kina mama wanaolea wanao peke yao yaani “President of Single Mothers” alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Aliangazia safari yake kama mzazi, kuachana na wanawe ambao sasa ni watu wazima na wanaishi kivyao na msongo wa mawazo unaotokana na hatua hiyo.

Mwimbaji huyo anajiandaa kwa harusi ya binti yake Fancy Makadia na amehakikishia wanawe kuhusu mapenzi aliyonayo kwao.

“Sikuwahi kufikiria kwamba siku itafika ambapo nyinyi wote mtakuwa watu wazima na kuondoka chini ya malezi yangu,” aliandika Akothee akiongeza kwamba hakutarajia kwamba siku moja angechagua kuishi Ulaya lakini maamuzi ya wanawe yamefikisha huko.

Nyota huyo alifichua kwamba watoto wake wa kiume ambao ndio wa mwisho hawana mipango ya kurejea Kenya isipokuwa wakati wa likizo za shule uamuzi ambao umemfanya naye ahamie Ulaya.

Mama huyo wa watoto watano amesema kwamba sasa atalazimika kujifunza kifaransa ndiposa aweze kuhusiana vyema na mashemeji zake na wajukuu wake watarajiwa.

Akothee amesema kwamba sasa anachohitaji ni usimamizi wa kuaminika wa shule aliyoanzisha ya Akothee Academy akisema mambo mengine anaweza kuyasimamia kutoka atakapokuwa.

“Nitawakosa sana mashabiki wangu lakini ninaamini kwamba nimetimiza kusudi langu nchini Kenya.” alimalizia msanii huyo.  Alishangaa ni lini wafuasi wake watamwandalia  sherehe ya kumuaga.

Share This Article