Mwanahabari wa shirika la Standard Group Zubeidah Kananu, amehifadhi kiti cha Rais wa chama cha Wahariri wa Habari nchini almaarufu Kenya Editors Guild(KEG).
Kananu amezoa kura 72 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Yvonne Okwara kutoka runinga ya Citizen, aliyepata kura 58, kwenye uchaguzi ulioandaliwa leo Jumamosi.
Francis Openda amechaguliwa naibu Rais huku Mhariri wa habari za redio katika shirika la KBC Agnes Mwangangi, akichaguliwa mwanachama wa kamati ya wahariri wa redio.
Julius Bosire amechaguliwa mwanachama wa masomo huku Milicent Awuor pia kutoka KBC, akichaguliwa mwakilishi wa runinga, wakati Linda Bach akichaguliwa mwakilishi wa habari za Gazeti, naye Kenfrey Keberenge akiwa mwakilishi wa wanahabari wa mitandaoni.
Martin Masai, Ruth Nesoba na Mbugua Ng’ang’a wamechaguliwa kuwa wanachama wa bodi ya usimamizi.
Uchaguzi huo uliokuwa uandaliwe Aprili 12 uliahirishwa kutokana na kukosekana kwa akidi ya wanachama.