Washukiwa wanne wa ujambazi wakamatwa, bunduki tatu zapatikana

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa wa ujambazi wakamatwa kaunti ya Nairobi.

Washukiwa wanne wa ujambazi wakiwemo raia watatu wa Uganda na Mkenya mmoja, wamekamatwa, huku bunduki tatu zikipatikana katika operesheni ya kiusalama iliyotekelezwa katika mitaa ya Dandora, Saika, Pumwani na Huruma Jijini Nairobi.

Operesheni hiyo ya Alhamisi Mei 23, 2025, ilifanywa baada ya visa kadhaa vya ujambazi kuripotiwa Jijini Nairobi na Magharibi mwa nchi.

Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), walianzisha msako dhidi ya majambazi wanne, na kuwakamata wote wakiwa na bastola, bunduki aina ya AK47 na risasi 50.

Wanne hao ni Sipholi Sam Wafula almaarufu Sande, Ogomba Alex, Mohammed Musa na Wafula Clinton.

Sipholi ndiye alikuwa wa kwanza kukamatwa na baada ya kuhojiwa aliwapeleka maafisa wa usalama katika nyumba yake mtaani Saika ambapo bastola aina ya Falcon ikiwa na risasi 11 ilipatiokana.

Naye Ogomba Alex alikamatwa katika nyumba yake mtaani Dandora ambapo alipatikana na bunduki aina ya  AK47 ikiwa na risasi 30.

Baada ya kuhojiwa washukiwa hao wawili waliwapeleka maafisa hao wa polisi katika nyumba ya Mohammed Musa mtaani Huruma, ambako alikuwa akiishi na familia yake, na ilibainika yeye ndiye mmiliki wa bunduki hiyo ya AK47.

Kupitia ukurasa wa X, idara DCI ilisema kuwa uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa raia hao watatu wa Uganda walirejea hapa nchini Mei 21, 2025 kupitia mpaka wa Malaba, baada ya kutoroka hapa nchini walipotekeleza uhalifu mtaani Kisii.

Aidha kulingana DCI,  Wafula Clinton (raia wa Kenya), anayeishi mtaa wa Githurai anayeaminika kuwa kiongozi wa genge hilo, alikamatwa mtaani Pumwani.

Wanne hao kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Starehe, wakisubiri kufikishwa mahakamani.

TAGGED:
Share This Article