Wakulima wa Nyandarua wapinga ripoti ya viazi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton

Jared Ombui
3 Min Read
Shamba la viza huko Nyandarua

Wakulima kutoka Wadi ya Nyakio, eneo la South Kinangop katika Kaunti ya Nyandarua, wamepinga vikali ripoti iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Egerton kuhusu matumizi ya viuatilifu kwenye kilimo cha viazi, wakikishutumu chuo hicho kwa kuwaacha nje kwenye utafiti na kuchapisha taarifa za kupotosha.

Wakulima hao waliokuwa na hasira, walizungumza katika mkutano wa kijamii na kusema kuwa hawakuwahi kushauriwa wala kuulizwa maswali yoyote wakati wa ukusanyaji wa data, na hivyo kutia shaka uhalali wa utafiti huo.

“Hakuna mtu aliyekuja shambani kwetu kutuuliza kuhusu viuatilifu tunavyotumia. Hii utafiti ilifanyika wapi basi, kama si kwenye mashamba yetu?” aliuliza mmoja wa wakulima, akiashiria hofu kwamba ripoti hiyo inalenga kudhoofisha biashara yao ya kilimo cha viazi.

Walisema kuwa kilimo cha viazi ndicho chanzo chao kikuu cha mapato, kinachowasaidia kulipia ada za shule za watoto wao, mahitaji ya afya na maisha ya kila siku. Wakulima hao waliitaka Egerton na taasisi nyingine za utafiti kushirikiana nao moja kwa moja kabla ya kutoa ripoti zinazoweza kuathiri maisha yao.

“Hii si ripoti tu – ni maisha yetu yanayowekwa rehani. Tunafanya kazi kwa bidii kila msimu kulisha taifa hili,” aliongeza mkulima mwingine.

Malalamiko yao yaliungwa mkono na Gavana wa Nyandarua, Dkt. Moses Kiarie Badilisha, ambaye aliikashifu ripoti ya Chuo Kikuu cha Egerton kama “tata, isiyo na msingi wa kisayansi na inayopotosha kabisa.”

Gavana Badilisha alikosoa mbinu zilizotumika katika ripoti hiyo na kuwalaumu watafiti kwa kushindwa kuwahusisha wadau muhimu kama vile mashirika ya serikali na wakulima wa eneo hilo. Alisema hatua hiyo inaleta maswali mengi kuhusu uaminifu na madhumuni ya ripoti hiyo.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa suala nyeti kama hili lilishughulikiwa kwa uzembe bila kuwahusisha mamlaka za eneo. Njia hii ya kufanya mambo inaleta taharuki isiyo ya lazima na inaweza kuharibu sifa ya kaunti,” alisema.

Alisisitiza kuwa Kaunti ya Nyandarua inashirikiana kwa karibu na Bodi ya Kudhibiti Bidhaa za Viuatilifu (PCPB) kuhakikisha matumizi salama ya viuatilifu. Pia alitaja mafunzo ya mara kwa mara kwa wakulima na uzalishaji wa mbegu bora na safi za viazi kama hatua muhimu ya kulinda afya ya walaji na kipato cha wakulima.

Aliwahimiza watafiti kushirikiana na serikali za kaunti pamoja na jamii kabla ya kutoa ripoti ambazo zinaweza kuathiri vibaya eneo zima.

“Nyandarua ni moja ya wazalishaji wakuu wa viazi nchini Kenya. Tumewekeza pakubwa katika kisasa na kitaalamu kwa kilimo, na hatutaruhusu ripoti zisizo na msingi kuhujumu juhudi za wakulima wetu,” aliongeza.

Share This Article