Rais William Ruto amesema serikali itaendelea kufanya kazi na mashirika mengine ili kutimiza ajenda yake ya mabadiliko.
Akizungumza leo Alhamisi alipokutana na Baraza Kuu la Kitaifa la shirika la Maendeleo ya Wanawake linaloongozwa na Rahab Mwikali Muiu katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema ushirikiano huo ni muhimu kwa ufanisi wa mipango ya serikali ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Huduma ya Afya kwa Wote, na kuwezesha jamii kupitia utoaji wa maji.
“Serikali itaendelea kufanya kazi na Shrika la Maendeleo ya Wanawake na mashirika mengine ili kuafikia ajenda ya mageuzi pamoja na kutekeleza huduma ya afya kwa wote UHC,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alipongeza Shirika hilo la Maendeleo ya Wanawake, akisema kwa muda wa miaka mingi limetoa mchango mkubwa katika kuwawezesha wanawake wa ngazi ya chini kote nchini.
“Shirika la Maendeleo ya Wanawake kwa muda wa miaka mingi limetekeleza wajibu muhimu kuwawezesha wananawake hapa nchini,” alidokeza Rais Ruto.