Wabunge wa Kenya na wawakilishi wa wizara ya fedha wanajiandaa kuhudhuria warsha ya siku tano kuhusu ufadhili wa mipango ya kukabili mabadiliko ya hali ya anga nchini.
Warsha hiyo itakayoandaliwa Mei 22 hadi 27, 2025 itaangazia pia jukumu la bunge katika kushughulikia changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo ambao umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya bunge na wizara ya fedha utasaidia wabunge kuelewa zaidi masuala ya tabianchi ili kuhakikisha wanaunga mkono mpango wa ufadhili wa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mpango huo wa ufadhili unaungwa mkono na washirika wa kimataifa kama vile benki ya dunia na serikali ya Kenya.
Chini ya uenyekiti wa Seneta Moses Kajwang’ na mbunge Charity Kathambi, warsha hiyo itaendeleza maudhui kutoka kwa kongamano kuhusu mabadiliko ya tabianchi almaarufu COP29 kwa kusisitiza haja ya ushirikishi zaidi wa bunge.
Masuala mengine yatakayoangaziwa humo ni pamoja na namna bunifu za kufadhili mipango ya mabadiliko ya tabianchi, utungaji wa sera na mikakati inayolenga kukidhi mahitaji ya maeneo husika.
Wabunge wataangazia pia njia za uangalizi na za kuimarisha ushirikishaji wa umma katika utawala wa tabianchi kwa lengo la kukuza mtandao hai na wenye ufahamu kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Wahusika wa warsha hiyo wanatarajia kupata ufahamu zaidi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake na uelewa wa kina kuhusu mbinu tofauti zilizoko za kufadhili hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.