Mwanamuziki na mwigizaji wa Marekani Jennifer Lopez ameshtakiwa kwa kuchapisha picha alizopigwa na Paparazzi alipokuwa akihudhuria sherehe ya Hollywood, kwa kukiuka hakimiliki.
Lopez alichapisha picha hizo zinazomwonyesha akiwasili kwenye studio za Amazon na sherehe ya Vanity Fair huko Los Angeles kwenye akaunti yake ya Instagram.
Sherehe hiyo ilifanyika usiku uliotangulia siku ya tuzo za Golden Globes mwezi Januari mwaka huu. Alikuwa amevaa rinda la rangi nyeupe na koti la manyoya la rangi nyeupe na alizichapisha kwenye Instagram na X.
Mpiga picha Edwin Blanco na shirika analofanyia kazi la Backgrid, wamemshtaki Jlo kila mmoja kivyake wakidai umiliki wa picha hizo mbili.
Katika mawasilisho yao wanadai kwamba Lopez alitumia picha zao kujiongezea ufuasi mitandaoni, akaongeza uwezekano wa picha hizo kusambazwa zaidi na kufanya machapisho yake yaaminike zaidi.
Backgrid na Blanco wanataka walipwe fidia ya dola elfu 150 kwa kila picha yao iliyotumika.
Kulingana nao matumizi ambayo hayakuwa yameidhinishwa ya picha hizo ni ya manufaa ya kiuchumi kwa msanii huyo, wakitoa mfano wa kutangaza bidhaa alizokuwa amevaa kama nguo na vipuli na hivyo kusaidia watengenezaji kupata mauzo zaidi.
Wanaelezea pia kwamba anayeonekana kwenye picha huwa sio mmiliki wa picha bali inamilikiwa na mpiga picha au kampuni ya upigaji picha.
Stakabadhi za kesi hiyo zinasema kwamba Backgrid na Blanco waliwasiliana na wawakilishi wa Jlo kuhusu matumizi ya picha zao na wakakubaliana kuhusu malipo ambayo hayakufanywa.
Hii sio mara ya kwanza Lopez anajipata katika hali hii, mwaka 2019 na 2020 alichukuliwa hatua kwa kutumia picha zake ambazo zilipigwa na watu wengine.