Nairobi City Thunder ilipoteza mechi yake ya tatu mtawalia ya ligi ya mpira wa kikapu barani Afrika kanda ya Nile baada ya kushindwa alama 75-74 na MBB ya Afrika Kusini katika uwanja wa ndani wa BK ,jijini Kigali, Rwanda.
MBB ilishinda robo ya kwanza vikapu 22-15 lakini Thunder iliyoongozwa na mchezaji mahiri Tylor Ongwae ilijizatiti na kushinda robo ya pili 18-10 na kuongoza kwa vikapu 33-32 ilipofikia wakati wa mapumziko.
Thunder iliendeleza umahiri wake katika kipindi cha tatu ilichotwaa pointi 27-18, Lakini MBB ilirejea mchezoni katika robo ya nne na kuifunga Thunder vikapu 25-14 na kupata ushindi,japo finyu wa alama 75-74.
Ushindi huo ulikuwa ni wa kwanza wa MBB kati ya mechi tatu iliyocheza katika mashindano hayo ya BAL ilhali Thunder inayoongozwa na kocha mkuu Bradley Ibs haijashinda mechi yoyote katika mashindano hayo yanayooandaliwa kwa mfumo wa ligi.
Ushinde unaiwacha Thunder na kazi ngumu ya kushinda michuano yake mitatu iliyosalia ili ifufue matumaini ya kufuzu fainali ya ligi hiyo mwezi ujao jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Thunder itamenyana na Al Ahli Tripoli alhamisi kabla ya kucheza na MBB jumamosi kisha ihitimishe michuano hiyo dhidi ya wenyeji APR jumapili.Timu mbili za mwanzo zitafuzu fainali hizo za Ligi ya mpira wa kikapu jijini Pretoria mwezi ujao.