Kenya inatarajiwa kuwa kitovu cha Utalii Barani Afrika, huku ikijiandaa kuwa mwenyeji kwa wajumbe 6,500 kutoka mataifa 40, watakaohudhuria mkutano wa 15 wa Magical Kenya Oktoba 1 hadi 3, 2025.
Makala ya mwaka huu yatavutia wanunuzi wa kimataifa wa hali ya juu, huku wafanyabiashara 400 wakionyesha bidhaa zao kwa siku tatu zitakazoshuhudia mazungumzo kuhusu uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.
Akizungumza wakati wa mkutano wa washikadau, katibu wa idara ya Utalii John Ololtuaa, alielezea umuhimu wa maonyesho hayo katika kubadilisha sekta ya Utalii Barani Afrika.
“MKTE 2025 sio tu ya kufurahiwa nchini Kenya, lakini inaashiria hatua kubwa barani humu,” alisema Ololtuaa.
Aidha katibu huyo alitoa wito kwa wadau katika sekta ya Utalii kutoangazia tu ushindani, lakini pia kukumbatia ushirikiano wa nje ya nchi.
“Tunapaswa kuwachukulia majirani wetu kama washirika lakini sio kama washindani. Utalii unasalia kuwa nguzo muhimu katika chumi zetu. tunaweza fanikisha uwezo kamili wa Afrika,” aliongeza katibu huyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Utalii June Chepkemei, alidokeza kuwa uvumbuzi utachukua sehemu muhimu katika hafla hiyo.
“Tunakumbatia teknolojia katika kila sehemu ya maonyesho haya, kuhakikisha uwajibikaji katika usimamizi wa maonyesho hayo,” alisema Chepkemei.