Polisi nchini Tanzania wameanzisha uchunguzi ili kubaini waliosambaza habari za uongo na za kupotosha kwenye mtandao wa X ambao awali ulifahamika kama Twitter.
Katika taarifa msemaji wa wa Jeshi la Polisi la Tanzania alisema, “Jeshi la Polisi linapenda kuwajulisha umma kuwa kuna taarifa za uongo, upotoshaji na zisizo na maadili zilizokuwa zikisambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Jeshi la Polisi (tanpol) kwa lengo la kutaka kuuaminisha umma kuwa zimetolewa na Jeshi la Polisi kupitia mtandao wake wa X.”
Hii ni baada ya akaunti rasmi ya jeshi hilo la polisi kudukuliwa na watu wasiojulikana ambao walichapisha habari mbaya kuhusu Tanzania.
Inaonekana kwamba jeshi hilo limefanikiwa kurejesha udhibiti wa akaunti hiyo kabla ya kuchapisha taarifa hii kwa umma.
Msemaji wa polisi alifafanua kwamba taarifa hizo si za kweli na kwamba Jeshi la Polisi haliwezi kuandaa na kusambaza taarifa kama hizo katika Mitandao yake ya kijamii.
“Wakati tunaendelea kufuatilia Wahalifu waliotengeneza na kusambaza taarifa hizo wakamatwe, tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo na kuepuka kuendelea kuzisambaza endapo zitakufikia” iliendelea kusema taarifa hiyo.
Polisi wameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote yule aliyehusika na utengenezaji na utoaji wa tarifa hizo. Wanaoendelea kusambaza taarifa hizo ambazo kufikia sasa zimefutwa pia wameonywa.