Gavana Natembeya akanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yake

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya afikishwa mahakamani.

Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya, amekanusha mashtaka ya ufisadi dhidi yake, alipofikishwa katika mahakama ya Milimani leo Jumanne.

Gavana huyo alishtakiwa kwa kupokea zawadi za kifedha kutoka kwa kampuni zilizofanya biashara na kaunti ya Trans Nzoia kati ya Januari 2023 na Aprili 2024.

Anadaiwa kupokea shilingi Milioni 1.1 kutoka kwa Mercy Chelangat, ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Lyma Agro Science Limited na ile ya Maria Stores, ambazo zimeripotiwa kufanya biashara na serikali ya kaunti ya Trans Nzoia.

Aidha Natembeya anadaiwa kupokea shilingi Milioni 2.1 kutoka kwa Emmanuel Wafula Masungo, mmiliki wa kampuni ya Easterly Winds ambayo pia inadaiwa ilifanya biashara na kaunti hiyo.

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi  (EACC) inadai kuwa Natembeya  alipokea kitita cha shilingi Milioni 3.25 million, kama sehemu ya malipo iliyotolewa na kaunti hiyo kwa kampuni ya Chelangat.

Kiongozi wa mashtaka amepinga kuachiliwa kwa dhamana kwa Natembeya, akisema huenda akavuruga uchunguzi unaoendelea pamoja na mashahidi.

Gavana huyo alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) siku ya Jumatatu katika makao yake ya Nairobi kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Ghasia zilizuka katika makazi yake ya Kitale wakati maafisa hao wa EACC waliokuwa wakitekeleza operesheni, kushambuliwa na kundi la watu. Magari kadhaa yaliharibiwa wakati wa purukushani hilo.

Share This Article