Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama za Milimani leo Jumanne, baada ya maafisa wa Tume ya Maadili na kukabiliana na Ufisadi EACC kumkamata siku ya Jumatatu kwa madai ubadhirifu wa shilingi bilioni 1.4.
Kundi la pamoja la maafisa wa EACC na wale wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, walifanya msako nyumbani kwa Gavana huyo katika mtaa wa Milimani, Kitale, kaunti ya Trans Nzoia Jumatatu asubuhi. Wakati wa msako huo Natembeya hakuwa nyumbani kwake.
Gavana huyo atashtakiwa kwa kushiriki ufisadi pamoja na Afisa Mkuu wa Fedha Emanuel Masungo, Dorothy Nyukuri Afisa Mkuu wa Maji, Eliyah Liambula Mkurugenzi wa ununuzi na Desmond Shivachi mwanakandarasi ambaye ni mwandani wa Gavana huyo.
Natembeya alikamatwa katika makao yake ya Nairobi siku ya Jumatatu na kuhojiwa katika Makao Makuu ya EACC, akisubiri kufikishwa mahakamani.