Chama cha United Democratic Alliance (UDA), kimemfurusha Seneta Mteule Gloria Orwoba kutokana na madai ya kukiuka maadali ya chama hicho.
Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar, amethibitisha kuwa kamati ya nidhamu ya chama hicho imeamua kumuondoa Orwoba chamani, baada ya kujadili swala hilo kwa kina.
Kulingana na Omar, hatua hiyo ilichukuliwa kuambatana na sehemu ya 29 ya katiba ya UDA na kurasimishwa na Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama hicho wakati wa mkutano ulioandaliwa Jumatatu May 19, 2025.
“Seneta Gloria Orwoba sasa sio mwanachama wa UDA . Hana ruhusa ya kuwakilisha au kutekeleza jambo kwa niaba ya chama katika wadhifa wowote,” alisema Omar.
Aidha Omar alidokeza kuwa chama cha UDA kimemuandikia rasmi Spika wa bunge la Senate ili kuanzisha mchakato wa kumuondoa Orwoba, na kimemteua Consolata Wabwire Wakwabubi kutoka eneo bunge la Kimilili, kaunri ya Bungoma kuchukua nafasi yake.
“Chama hiki kimemfahamisha Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhusu kutimuliwa kwake,” aliongeza Omar.
Mnamo Aprili 17,2025, Orwoba alikuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kumlaki waziri wa zamani Fred Matiang’i aliyewasili nchini na baadaye alihudhuria sherehe ya kumkaribisha katika uwanja wa Gusii Mei 2, 2025, hatua ambayo UDA inachukulia kuwa usaliti.