Msanii wa muziki nchini Marekani Chris Brown atendelea kuwa rumande nchini Uingereza hadi Juni 13, 2025 wakati atarejeshwa mahakamani.
Brown alinyimwa dhamana na Jaji Joanne Hirst wa mahakama ya Southwark Crown jijini London Ijumaa Mei 16, 2025 katika kesi inayomkabili ya kusababishia mtayarishaji wa muziki madhara mwilini, kisa kilichotokea mwaka 2023.
Februari 19, 2023, Brown alimshambulia Abe Diaw ndani ya klabu cha burudani katika wilaya ya Mayfair wakati wa majibizano kati yao akitumia chupa ya pombe ambayo alimgonga nayo kichwani.
Alishtakiwa kwa kosa la kumsababishia mtayarishaji muziki huyo madhara mwilini kimakusudi na kulingana na sheria za Uingereza hilo ni kosa kubwa.
Mwanamuziki huyo alikuwa amekwenda Uingereza kwa ajili ya ziara ya kikazi na alikamatwa Mei 15, 2025 katika hoteli ya Lowry iliyoko Manchester.
Hatima ya ziara yake ya kimuziki sasa haijulikani hatua inayowaacha mashabiki wake katika hali ya wasiwasi. Ziara hiyo aliyoipa jina la “Breezy Bowl XX” ilistahili kuanza Juni 8, 2025 huko Uholanzi.