Naibu Rais Kithure Kindiki amesisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa, amani na mabadiliko ya kiuchumi kuanzia kwa watu wa tabaka la chini, wakati wa ziara yake huko Amagoro na eneo bunge la Gatundu Kusini kaunti ya Kiambu.
Akizungumza wakati wa ibada ya madhehebu mbali mbali katika uwanja wa shule ya msingi ya Amagoro, Teso Kaskazini kaunti ya Busia, Kindiki alitoa hakikisho kuhusu kujitolea kwa serikali ya Kenya Kwanza kuhakikisha maendeleo kila sehemu ya nchi.
Kiongozi huyo alionya viongozi dhidi ya siasa za migawanyiko kwa misingi ya kabila akisema, “Tunawakilisha umoja, uthabiti na kutogawanyika kwa nchi yetu.”
Aliwazomea viongozi wa kisiasa na wa kidini ambao huzua migogoro ya kikabila akiwataja kuwa wasio wazalengo na wanaoendeleza mambo yaliyopitwa na wakati.
Kindiki alisisitiza kwamba serikali inaangazia mipango ya kuleta mabadiliko nchini kama kilimo,elimu, afya na miundombinu kwa lengo la kuinua jamii za mashinani.
Alipongeza taasisi za kidini kwa jukumu lao kubwa katika kuchangia maendeleo ya kitaifa. Naibu Rais alikuwa ameandamana na waziri wa mazingira Deborah Barasa na wabunge wa eneo hilo akiwemo Oku Kaunya wa TesoKaskazini na Mary Emase wa Teso Kusini.
Baadaye katika eneo la Gatundu Kusini alihakikishia wakenya kwamba uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa amani na akaonya wanasiasa dhidi ya matamshi mabaya.
Kulingana naye, matamshi ya kubashiri vurugu wakati wa uchaguzi ni tabia ya watu wasio wazalendo na ni hatari huku akiapa kutokubali nchi irejelee vita vua kisiasa.
Kindiki alipigia debe ajenda ya mageuzi ya kiuchumi almaarufu Bottom-Up Economic Transformation Agenda – BETA, akitaja miradi iliyotekelezwa chini yake kufikia sasa kama masoko ya kisasa 400 na mpango wa ufadhili wa biashara ndogo wa Nyota.