Serikali imetangaza kutekeleza mageuzi katika vyama vya ushirika,katika juhudi mpya za kufufua sekta ya pamba hapa nchini.
Katibu katika wizara ya Vyama vya Ushirika Patrick Kilemi, amesema mswada wa sheria ya ushirika wa 2024, ambao kwa sasa uko katika bunge la Seneti, unanuia kuondoa ufisadi, usimamizi mbaya na makundi haramu ambayo yametatiza sekta hiyo kwa muda mrefu.
Akizungumza afisini mwake, katibu huyo alisisitiza sheria hiyo mpya italainisha operesheni katika vyama vya ushirika kwa kubuni muda wa kuhudumu kwa maafisa na kuwafurusha walaghai wanaojisingizia kuwa wafanyakazi wa Vyama vya Ushirika.
“Siku za walaghai na maafisa wafisadi zimefikia kikomo. Mswada wa Vyama vya Ushirika wa mwaka 2024, utaleta nidhamu katika sekta ya pamba,” alisema Kilemi.
Matamshi yake yanawadia huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kutoka kwa wakulima katika maeneo yanayokuza kilimo cha pamba,kama vile Lamu, Busia, na Siaya, ambapo mbegu za pamba zinazosambazwa na serikali zinaripotiwakuuzwa kwa bei ghali, na maafisa wa vyama vya ushirika wafisadi.
Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda 5 vipya vya katika maeneo muhimu yanayokuza zao la pamba. Miongoni mwa viwanda vinayojengwa ni ile ya Mpeketoni kaunti ya Lamu ambayo ndio kaunti inayokuza pamba kwa wingi hapa nchini.