Harmonize amwachilia Chinga

Ibraah amekuwa akitaka kuondoka kwenye kampuni ya Harmonize ya Konde Music lakini hakuweza kutimiza mahitaji ya mkataba.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Konde Music Worldwide Harmonize ametangaza kwamba amemwachilia msanii Ibraah au ukipenda Chinga ambaye amekuwa chini ya usimamizi wa kampuni yake.

Katika video aliyochapisha Instagram leo asubuhi, Harmonize alisema amemwachilia Ibraah na kuanzia leo ni msanii huru huku akihimiza waandaaji wa matamasha wawe wakimpa fursa.

Kuhusu chanzo cha mvutano wa mtandaoni kati yao, Harmonize alielezea kwamba Chinga alimtumia ujumbe akisema anataka kuondoka Konde Music. Hapo ndipo alimshauri aketi na wasimamizi wa kampuni wakamilishe mahitaji ya mkataba kisha aondoke.

Alielezea kwamba kulingana na mkataba ambao Ibraah alitia saini miaka minne iliyopita, anahitajika kulipa kiasi cha pesa alichokitaja ili kumiliki kikamilifu kazi zake za muziki alizotengeneza akiwa Konde Music.

Harmonize alizungumzia pia hatua yake ya kukosa kufika katika kikao kilichoitishwa na Baraza la Sanaa la Taifa ambapo alielezea kwamba hakuona kama kulikuwa na zogo la kusuluhishwa kati yake na Ibraah anatemrejelea kama mdogo wake.

Anasema alituma wawakilishi kutoka kampuni ya Konde Music kuhudhuria kikao hicho.

Kama kaka mkubwa amemsamehe Ibraah kwa mambo yote aliyomrushia mitandaoni ya kumchafulia jina akisema sio ya kweli na wala hahitaji amwombe msamaha.

Katika maelezo chini ya Video yake, Harmonize alisema kwamba kampuni ya Konde Music itatoa taarifa rasmi kuhusu uamuzi wake wa kumwachilia Ibraah.

Share This Article