Usimamizi wa maduka ya jumla ya Naivas umekanusha madai ya kufungwa kwa matawi yake ya Nairobi kutokana na kile kilichotajwa kuwa uuzaji wa bidhaa zilizoharibika.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, usimamizi huo ulipuuzilia mbali madai hayo na kuyataja kuwa ya uwongo, ya kupotosha na yenye athari mbaya.
Kampuni hiyo inahakikishia umma na wateja wake kwamba hakuna bidhaa ambazo tarehe ya matumizi imepita zimepatikana humo na kwamba matawi yake yote yanaendelea kuhudumu kama kawaida kote nchini.
Naivas ilisisitiza kujitolea kwake kudumisha viwango vya ubora na uzingatiaji kama inavyohitajika na viwango vya afya na usalama.
“Matawi yetu yote yanaendelea kuhudumu kama kawaida na yanazingatia viwango vya kitaifa na vya kaunti vilivyowekwa na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini KEBS, wizara ya Afya na mashirika husika” ilisema taarifa hiyo.
Naivas ilifichua pia kwamba inatafuta ushauri wa kisheria kuhusu hatua inazofaa kuchukua dhidi ya walioanzisha na kusambaza uvumi huo huku ikisisitiza kuhusu sera yake ya kutokubali kamwe utoaji na utozaji hongo.
Wateja ambao wanataka ufafanuzi zaidi wamehimizwa kuwasiliana na idara ya mahusiano ya wateja ya Naivaskupitia nambari ya sumu 0202329801 au barua pepe anwani ikiwa customerservice@naivas.co.ke.