Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini Kenya vinaendelea huku mamlaka ya kitaifa ya kupambana na matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya – NACADA ikitekeleza oparesheni mbili kubwa katika kaunti za Homabay na Kisii.
Katika oparesheni hizo dawa haramu zilinaswa na washukiwa kadhaa kukamatwa.
Katika mji wa Oyugis ambao uko katika kaunti ya Homabay, oparesheni ya pamoja iliyoongozwa na NACADA, Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ANU) na Huduma ya Polisi wa Utawala (APS) ilisababisha kukamatwa kwa watu wawili.
Walipatikana na bidhaa haramu zikiwemo pakiti 400 za sigara aina ya Supermatch ambazo hazikulipiwa ushuru, pakiti 14 za sigara aina ya Oris na bangi.
Fedha taslimu za thamani mbalimbali pia zilinaswa, zikiaminika kuwa mapato kutokana na biashara hiyo haramu. Washukiwa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oyugis huku uchunguzi ukiendelea.
Katika Kijiji cha Nyakongo, Kaunti ya Kisii, msako mwingine uliofanywa katika makazi fulani ulisababisha kupatikana kwa fagio 134 zinazoshukiwa kuwa na dawa za kulevya na magunia mawili ya kilo 90 yaliyokuwa na majani makavu yanayodhaniwa kuwa bangi.
Washukiwa wanane walikamatwa na wanashikiliwa na polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Msako huo unafuatia kuvunjwa kwa mtandao mkubwa wa usambazaji wa dawa za kulevya uliohusishwa na mfanyabiashara maarufu wa mihadarati huko Kisii mwezi mmoja uliopita, hatua inayodhihirisha azma ya NACADA kuendeleza mapambano dhidi ya mihadarati.
Msemaji wa NACADA alisema oparesheni hizi ni dhihirisho la dhamira ya mamlaka hiyo ya kuvuruga mitandao ya biashara ya dawa za kulevya na kulinda jamii.
Alisisitiza kwamba wataendelea kushirikiana katika ujasusi na mashirika mengine ya usalama, huku akihimiza wananchi kuendelea kuwa waangalifu na kuripoti shughuli zozote zinazohusiana na dawa za kulevya.
Wanaweza kufanya hivyo kwa njia ya siri kupitia nambari 1192, isiyotozwa malipo yoyote.