Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA nchini Tanzania, limeingilia kati mzozo wa mwanamuziki Ibraah na kampuni inayomsimamia ya Konde Music inayomilikiwa na msanii Harmonize.
BASATA ilichapisha bango kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa Instagram lililokuwa na picha ya Harmonize na ya Ibraah na maelezo kwamba imeingilia kati na kualika wawili hao wafike katika afisi zao.
Wasanii hao wawili wanafaa kufika kwenye afisi za BASATA leo Jumatatu Mei 12, 2025 saa mbili asubuhi.
Hata ingawa bango la BASATA halikuwa na sababu ya mwaliko wa wawili hao, inaaminika kwamba watajaribu kupatanisha wawili hao katika mzozo unaohusu nia ya Ibraah ya kuondoka Konde Music na pesa anazopaswa kulipa kabla ya kufanya hivyo.
Haya yanajiri muda mfupi baada ya Kampuni ya Harmonize Konde Music Worldwide kutangaza kwamba imemsimamisha rasmi msanii wake, Ibrahim Abdallah Nampunga maarufu kama Ibraah.
Tangazo hilo lilielezea kwamba Ibraah haruhusiwi kushiriki shughuli zozote za muziki kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wake na kampuni hiyo hadi pale utata unaomzunguka utakapotatuliwa kwa mujibu wa mkataba wake na sheria za Tanzania.
Haya yanafuatia hatua ya Ibraah ya kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii maneno ambayo yanamkosea heshima mmiliki wa kampuni inayomsimamia Harmonize.
Konde Music imempiga marufu kuchapisha, kutamka au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.
Ibraah alianza kwa kumlaumu Harmonize kwa kumtaka alipe shilingi bilioni moja ndiposa aondoke Konde Gang. Harmonize alifafanua kwamba sio yeye binafsi amemwomba Ibraah pesa hizo bali ni kulingana na mkataba aliotia saini.