Spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula amehimiza wakenya watoe maoni yao au malalamishi kuhusu walioteuliwa kuhudumu kwenye tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
Wetangula anawataka wakenya kutoa mawasilisho yao kwa kamati ya bunge la taifa kuhusu haki na sheria kabla haijaanza kuwasaili saba hao walioteuliwa kuwa mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
Akizungumza jana katika shule ya upili ya Mtakatifu Michael Kamelilo katika kaunti ya Nandi, Wetang’ula alisema Rais William Ruto anatekeleza tu mahitaji ya katiba kwa kuwasilisha majina ya wateuliwa hao bungeni.
Alisisitiza kwamba bunge ndilo litafanya uamuzi wa mwisho wa kukubali au kukataa wateuliwa hao.
Wakati huo huo viongozi wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza wanahimiza bunge la taifa liharakishe usaili na uidhinishaji wa wateuliwa hao wa IEBC.
Wakiongozwa na kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah na Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, viongozi hao walitetea mchakato wa uorodheshaji wa wawaniaji wa nyadhifa hizo na usaili wao wakisema ulitekelezwa kulingana na sheria.
Ichung’wa alisema Rais William Ruto alitekeleza jukumu lake kwa kumchagua Erastus Ethekon kama mwenyekiti wa IEBC na wengine sita kama makamishna.
Walisema kuidhinishwa kwa wateuliwa hao kutatoa fursa ya chaguzi ndogo kufanyika katika maeneo mbali mbali nchini.