Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano ametoa heshima kwa kina mama kote duniani kwa mchango wao muhimu katika kuinua familia na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Akizungumza wakati wa sherehe ya siku ya kina Mama katika kijiji cha Gwa Kihara, eneo bunge la Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua, Miano alisisitiza nafasi kuu wanayochukua kina mama katika kukuza upendo, umoja na mafungamano thabiti ya kifamilia.
Alieleza kuwa kina mama ni msingi wa jamii, wakifanya kazi kimya kimya nyuma ya pazia ili kuhakikisha ustawi na utulivu wa familia zao.
Kauli yake iliungwa mkono na mzee wa kijiji Wachira Njari, aliyefananisha kina mama na “aina ya kipekee” waliobeba jukumu la kuongoza watoto wao katika hatua za awali za maisha, ikiwemo kujifunza lugha.
“Kina mama ndio injini ya kuhifadhi lugha za mama na tamaduni zetu” alisema. “Kupitia kwao, utambulisho wetu wa lugha na utamaduni huendelezwa kizazi hadi kizazi.”
Njari aliongeza kuwa kina mama si walezi tu bali pia ni walimu wa kwanza wakifundisha maadili, simulizi za kitamaduni, na nguvu ya kihemko kwa watoto wao. Ushawishi wao, alieleza, unaenea zaidi ya familia na kugusa jamii nzima.
Miano alisisitiza umuhimu wa kuwezesha kina mama kupitia elimu na fursa za kiuchumi, akisema kuwa kufanya hivyo kunaimarisha jamii moja kwa moja na kuchangia maendeleo ya kitaifa.
Aliitaka jamii kuwaheshimu na kuwaunga mkono kina mama si tu katika siku ya kina mama pekee, bali kila siku, kutokana na nafasi yao ya kipekee isiyoweza kubadilishwa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo, wakazi na wanafunzi, ambao waliadhimisha siku hiyo kwa nyimbo na mashairi, wakitoa ishara ya shukrani kwa kujitolea kwa kina mama katika familia na jamii.