Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imekusanya ushuru wa shilingi Trilioni 2.112 kufikia Aprili 30, 2025, hii ikiashiria asilimia 96.5 ikilinganishwa na kiwango kilicholengwa cha shilingi Trilioni 2.189.
Katika kipindi hicho, ukusanyaji ushuru uliongezeka kwa asilimia 6.1, ikilinganishwa na shilingi Trilioni 1.990 zilizokusanywa katika kipindi sawa na hicho mwaka wa kifedha wa 2023/2024.
Kwenye kipindi hicho, ushuru wa nyumbani uliokusanywa ulifika shilingi Trilioni 1.386 kati ya mwezi Julai – Aprili 2024/25, kuashiria ukuaji wa mapato kwa asilimia 4.7 dhidi ya shilingi Trilioni 1.323 zilizokusanywa kati ya mwezi Julai hadi April mwaka wa kifedha wa 2023/24.
Mapato kupitia forodha pia yaliongezeka kwa asilimia 9.1 baada ya kukusanywa shilingi Bilioni 722.743, ikilinganishwa na shilingi Bilioni 662.447 zilizokusanywa katika kipindi sawa na hicho mwaka wa kifedha wa 2023/24.
Aidha, fedha zinazokusanywa kwa niaba ya asasi zingine za serikali, zilikuwa shilingi Bilioni 205.518 hii ikiwa ni asilimia 111.8 dhidi ya lengo lililowekwa la kukusanya shilingi Bilioni 183.789. Hii inaashiria ukuaji wa asilimia 37.1, ikilinganishwa na shilingi Bilioni 149.876, zilizokusanywa katika kipindi sawa na hicho katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Wakati huo huo fedha zinazokusanywa kwa niaba ya Hazina Kuu zilifika shilingi Trilioni 1.906, kuashiria ukuaji wa asilimia 95.0 dhidi ya kiwango kilicholengwa cha shilingi Trilioni 2.006. Hii inawakilisha ukuaji wa asilimia 3.6, ikilinganishwa na shilingi Trilioni 1.840 zilizokusanywa katika kipindi sawa na hicho katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024.