Kansiime kulengwa kwenye ‘Roast’ ya kwanza nchini Uganda kesho

Roast ni aina ya hafla ya vichekesho ambayo wachekeshaji hurusha maneno ya kejeli yenye kuchekesha kwa mtu au watu fulani maarufu na asili yake ni Marekani.

Marion Bosire
2 Min Read
Anne Kansiime

Mwigizaji na mchekeshaji wa Uganda Anne Kansiime atakuwa mhusika mkuu wa Roast ya kwanza kabisa nchini Uganda kesho Mei 9, 2025 katika hoteli ya Sheraton jijni Kampala Kesho.

Roast ni aina ya hafla ya vichekesho ambayo wachekeshaji hurusha maneno ya kejeli yenye kuchekesha kwa mtu au watu fulani maarufu na asili yake ni Marekani.

Anne Kansiime ndiye atakuwa akirushiwa vijembe hivyo katika hafla hiyo aliyoandaa iitwayo “The Comedy Grill of Anne Kansiime” na wachekeshaji na watu maarufu nchini humo.

Richard Tuwangye na Deedan Muyiira ndio watakaongoza kikao hicho cha vichekesho huku orodha ya wachekeshaji ikisheheni majina kama Salvador, Madrat na Chico. Watangazaji Gaetano Kagwa, Sheila Gashumba na Prim Asiimwe pia watamchoma Kansiime.

Wasanii Nana Kagga na GNL Zamba na waziri wa zamani Miria Matembe watahusika pia katika hafla hiyo ya vichekesho bila kusahau Omara Daniel na Abraham Tukahiirwa maarufu kama Skylanta ambaye alikuwa mume wa Anne Kansiime.

Kansiime ana imani kwamba waandishi wa mswada wa onyesho hilo la vichekesho ambao ni Hillary Okello na Emah Napoelone wamejiandaa vilivyo kuhakikisha watumbuizaji wanaleta mambo mazuri jukwaani.

“Hatubahatishi na hatutaki kukosa kuridhisha yeyote atakayekuja akitarajia aina fulani ya onyesho” alisema Kansiime.

Ada wastani ya kiingilio ya onyesho hilo ni shilingi 100,000 pesa za Uganda sawa na shilingi 3,500 za Kenya.

Share This Article