Bitange Ndemo ateuliwa Naibu Chansela UoN

Uteuzi wake ulithibitishwa kupitia barua ya Mei 2, 2025 iliyoandikwa na mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha Nairobi Profesa Amukowa Anangwe kwa waziri wa elimu Julius Ogamba.

Marion Bosire
2 Min Read

Profesa Elijah Bitange Ndemo ameteuliwa kuwa Naibu Chansela mpya wa chuo kikuu cha Nairobi – UoN.

Ndemo ambaye aliwahi kuwa katibu katika wizara ya teknolojia ya habari na mawasiliano na ambaye sasa ni balozi wa Kenya huko Ubelgiji anarejea katika nyanja ya elimu ya juu.

Uteuzi wake ulithibitishwa kupitia barua ya Mei 2, 2025 iliyoandikwa na mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha Nairobi Profesa Amukowa Anangwe kwa waziri wa elimu Julius Ogamba.

Hatua hii inadhihirisha mwamko mpya kwa taasisi hii ya kipekee ya taifa la Kenya ya elimu ya juu.

Katika barua yake, Profesa Amukowa alisema, “Mwenyekiti wa baraza la chuo kikuu cha Nairobi amemteua Profesa Elijah Bitange Ndemo kama Naibu Chansela wa chuo hiki” akielezea kwamba htua hiyo inastahili kuratibiwa na baraza hilo.

Anangwe alihimiza pia wizara ya elimu kuchukua hatua za haraka katika kuratibu uteuzi huo ili kuwezesha mabadiliko hayo.

Ndemo anatarajiwa kuchukuwa wadhifa huo baada ya kukamilisha muda wake wa kuhudumu kama balozi wa Kenya nchini Ubelgiji. Profesa Francis Mulaa ameteuliwa na baraza la chuo kikuu cha Nairobi kuwa kaimu Naibu Chansela kwa miezi sita.

Ndemo anafahamika kwa mabadiliko aliyoleta katika nyanja ya dijitali nchini Kenya alipokuwa katibu wa wizara ya teknolojia ya habari na mawasiliano mwaka 2005 hadi 2013.

Mafanikio yake katika kipindi hicho ni pamoja na ustawishaji wa mfumo wa Afrika Mashariki wa shughuli za baharini, mfumo ambao ulipunguza pakubwa gharama ya internet na mawasiliano ya simu za rununu nchini Kenya.

Share This Article