Waziri wa Afya Aden Duale alifanya mazungumzo na afisa mkuu wa ubalozi wa Marekani nchini Kenya Marc Dillard ambapo walikubaliana kuhusu haja ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya Afya.
Waligusia pia kuhusu haja ya kuhakiki misaada inayotolewa na Marekani kwa Kenya.
Majadiliano ya wawili hao yaliangazia upanuzi wa ushirikiano katika nyanja muhimu kama vile maendeleo ya wahudumu wa afya, mifumo ya kidijitali ya deta ya afya, magonjwa yasiyoambukizwa na afya ya akili.
Uhusiano wa tabianchi na afya pia ulikuwa sehemu ya nyanja zilizoangaziwa ambazo ni muhimu katika kuafikia ajenda ya utoaji wa huduma za afya kwa wote.
Duale alifurahikia ushirikiano endelevu kupitia ajenda ya ulimwengu ya usalama wa afya – GHSA inayosaidia kuimarisha mifumo ya afya, ufuatiliaji wa magonjwa na huduma za dharura.
Alitambua athari ya mipango inayofadhiliwa na Marekani kama vile PEPFAR, USAID na CDC, hasa katika kupambana na magonjwa kama ukimwi, kifa kikuu na malaria.
Waziri huyo wa Afya alitoa hakikisho la kujitolea kwa Kenya katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na maadili katika mipango yote ya pamoja ya afya.
Mwakilishi wa Marekani nchini Marc Dillard kwa upande wake alidhihirisha utayari wa nchi yake wa kufungamanisha usaidizi wake na mikakati ya afya ya Kenya ili kuimarisha mifumo ya afya nchini.
Waziri alikuwa ameandamana na mkurugenzi mkuu wa afya Patrick Amoth, mkurugenzi wa afya ya jamii Bashir Isaak na msimamizi mkuu wa NASCOP Andrew Mulwa.