Hatutajibizana tena na upinzani, asema Kimani Ichung’wa

Tom Mathinji
3 Min Read

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wa, amesema viongozi wanaoiunga mkono serikali kwa sasa, hawatajibizana kisiasa na upinzani bali wataelekeza juhudi zao kwenye masuala ya maendeleo.

Ichung’wa alisema viongozi wa upande wa serikali watatumia muda wao mwingi kuwaeleza wananchi mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana chini ya utawala wa serikali Kenya Kwanza.

“Tangu sasa hamtasikia tukizungumza kuhusu watu binafsi kama vile wapinzani wetu hufanya, ila tutakuwa tukizungumza kuhusu maendeleo yanayoendelea katika sehemu mbalimbali za nchi,” alisema Mbunge wa Kikuyu.

Ichung’wa alikuwa akizungumza katika mji wa Ol Jabet, kaunti ndogo ya Marmanet, Kaunti ya Laikipia, wakati wa hafla ya kuchangisha pesa kuwezesha vikundi mbalimbali, iliyoandaliwa na Mwakilishi wa Wanawake wa eneo hilo, Jane Kagiri.

Kagiri alisema mwaka 2024 ulikuwa mgumu kwa wabunge kwani walilazimika kufanya maamuzi ya kubaki upande wa serikali ili kupata maendeleo au kujiondoa na kukosa usaidizi.

Alisema aliamua kuendelea kuiunga mkono serikali kwa sababu Laikipia inahitaji msaada ili kukabiliana na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, ujenzi wa barabara, kuongezwa kwa mtandao wa umeme na upatikanaji wa maji kwa wakazi.

“Mwaka jana singeweza kwenda mahali ambapo hakuna pesa. Nitasalia serikalini hadi mizozo kati ya binadamu na wanyama wa porini ikomeshwe, barabara zijengwe, umeme uongezwe na maji yapatikane kwa watu wa Laikipia,” alisema Mwakilishi huyo wa Wanawake, ambaye pia alifichua nia yake ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo kufuatia mabadiliko ya hivi karibuni.

Mbunge Mteule Sabina Chege aliwasihi wazazi kuwashauri watoto wao vyema, akisema kuwa ni aibu mtu kumrushia Rais William Ruto kiatu huko Migori, kwani Rais ni ishara ya umoja wa taifa na anapaswa kuheshimiwa na kila mmoja.

Chege aliwataka wakazi wa Laikipia kukataa siasa mbaya zinazopigiwa debe na “watu fulani.”

Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu, Ann Wamuratha, alisema kuwa wabunge wanaounga mkono serikali wanafanya kazi kwa bidii kupinga uongo unaoenezwa na wapinzani.

“Tulifanya kosa mwaka jana kwa kuwaruhusu wapinzani kusambaza uongo uliosababisha hata kuvamiwa kwa bunge.

“Tunataka kukanusha uongo kuhusu SHA na ufadhili wa vyuo vikuu. Tunataka mujiunge na SHA, mpeleke watoto vyuoni kisha muulize maswali baadaye,” alisema Wamuratha.

Ichung’wa alitoa mchango wa Shilingi milioni moja na kuwasilisha Shilingi  milioni  tatu kutoka kwa Rais Ruto.

Wabunge Wachira Karani (Laikipia Magharibi) Sabina Chege na Ann Wamuratha walitoa Sh200,000 kila mmoja.

Share This Article