Rais wa Muungano wa Milki za Kiarabu – UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan amemtunuku Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan medali ya ‘Mother of the Nation Order’.
Rais Samia alipokezwa medali hiyo katika ikulu ya Dar es Salaam na naibu waziri mkuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa UAE Sheikh Abdullah Bin Zayed Al Nahyan.
Medali hiyo ambayo ni mojawapo ya medali kuu za uongozi wa UAE hukabidhiwa kiongozi ambaye ametoa mchango wa kuleta maendeleo endelevu kwa jamii yake.
Imetolewa kwa Rais wa Tanzania kama njia ya kutambua mchango wake mkubwa wa kuletea Watanzania maendeleo endelevu ambayo yanaendana na sera za UAE za maendeleo endelevu ya kijamii, uwezeshaji wanawake na ushirikiano wa kimataifa.
Sheikh Abdullah aliwasilisha pia salamu kutoka kwa Rais wa UAE huku akiwatakia kheri wananchi wa Tanzania katika maendeleo pamoja na ustawi zaidi.
Alisisitiza kuimarishwa zaidi uhusiano wa kudumu baina ya nchi hizo mbili na kusisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano katika sekta muhimu.