Yammi aondoka kwenye kampuni ya Nandy

Kampuni hiyo ya The African Princess Records ilitangaza hili kupitia taarifa rasmi jana.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Tanzania Yasirun Yasin Shaban maarufu kama Yammi ameondoka rasmi kwenye kampuni ya muziki na kusimamia wanamuziki ya The African Princess Records.

Kampuni hiyo inamilikiwa na Faustina Charles Mfinaga au ukipenda Nandy ambaye pia ni mwanamuziki.

Tangazo hilo lilitolewa Mei 5, 2025 kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari iliyoelezea kwamba Yammi amehitimisha rasmi mkataba wa usimamizi wa kazi zake na kampuni ya The African Princess.

Ilielezea kwamba waliafikia makubaliano ya kirafiki na kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kampuni hiyo iliendelea kusema kwamba kwa muda ambao alikuwa chini ya usimamizi wake, Yammi aling’aa kupitia kipaji chake kilichovutia wengi ndani na nje ya Tanzania.

“Tumeshuhudia mafanikio makubwa kupitia nyimbo zilizofanya vizuri, maonesho ya moja kwa moja na ukuaji wa umaarufu wake katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya” ilisema taarifa hiyo.

Kampuni ya Nandy inaamini kuwa ilitoa mazingira bora yaliyomwezesha Yammi kukua na kupevuka kama msanii na wanafurahia kwamba amepata wawekezaji wapya watakaoendeleza usimamizi wa kipaji chake.

Kufuatia kuondoka kwa Yammi, African Princess Records ina fursa ya kuendelea na dhamira yake ya kuinua wasanii wapya, kuwekeza kwao na kuendelea kuchangia katika maendeleo ya muziki wa Tanzania na Afrika.

Wasimamizi wa kampuni hiyo wanamtakia Yammi kila la heri katika safari yake mpya ya muziki.

Share This Article