Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 10, Agnes Jebet Ng’etich, aliibuka mshindi wa taji ya Grand Slam Track katika mbio za masafa marefu zilizokamilika jana mjini Miami,Marekani.
Jebet Ngetich, alimaliza wa tatu jana mjini Miami, katika mbio za mita 3,000 kwa dakika 8 sekunde 23.14, na alikuwa ameshinda mbio za mita 10,000, hivyo basi kutawazwa bingwa wa jumla baada ya kuzoa alama 18.
Ushindi huo ulimwezesha Jebet Ngetich kutuzwa shilingi milioni 13 .
Bingwa wa dunia Mary Mora, alishinda mbio za mita 800 kwa dakika 1 na sekunde 59.51, na kumaliza wa pili kwa jumla katika msururu wa mashindano hayo na kutuzwa shilingi milioni 6.5.
Mashindano hayo yalianzishwa na mwanariadha mstaafu wa Marekani katika mbio za masafa mafupi Michael Johnson.
Johnson alitawazwa bingwa mara nne wa Olimpiki na pia kunyakua mataji saba ya dunia.