Polisi na maafisa wa upelelezi wa jinai wanaohudumu katika kituo cha polisi cha Naivasha walikamata washukiwa saba wa ujambazi kufuatia taarifa walizopashwa na wananchi.
Washukiwa hao wanahusishwa na visa mbali mbali vya wizi wa kimabavu mjini Naivasha na maeneo ya karibu.
Polisi walipata bastola moja aina ya Retay Falcon kutoka kwa saba hao.
Patrick Handi wa umri wa miaka 45, David Muchina wa miaka 34, Grace Wanjiru wa miaka 33, Erick Kabiru wa miaka 32, Hassan Jamal wa miaka 32, Christopher Kimani wa umri wa miaka 30 na Ronny Muturi wa miaka 30 walikamatwa mjini Naivasha.
Walikuwa kwenye gari dogo aina ya Mazda Demio la rangi ya kijivu nambari ya usajili KCS 384B.
Baada ya msako polisi walipata bastola hiyo ambayo haina uwezo wa kurusha risasi lakini ndiyo imekuwa silaha ya majambazi hao.
Wamekuwa wakiitumia kutishia wakazi wa Naivasha wasiokuwa na hatia kabla ya kuwaibia mali zao na kisha kutoweka.
Maafisa wa polisi waliohusika katika oparesheni hiyo wamesema washukiwa hao wanaandaliwa kwa ajili ya kufikishwa mahakamani leo.