Mudavadi ahimiza umoja magharibi mwa nchi

Waziri huyo alihimiza viongozi pia waweke kando tofauti zao na kuangazia mustakabali wa pamoja wa kisiasa.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi amehimiza jamii ya eneo la magharibi mwa Kenya kuungana na kuunga mkono Rais William Ruto atakapokuwa aitafuta kuchaguliwa kwa muhula wa pili mwaka 2027.

Mudavadi ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni alikuwa akizungumza katika kaunti ya Vihiga kwenye hafla ya uwezeshaji iliyoandaliwa na mwakilishi wa kaunti hiyo bungeni Beatrice Adagala.

Waziri huyo alihimiza viongozi pia waweke kando tofauti zao na kuangazia mustakabali wa pamoja wa kisiasa.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa eneo la magharibi akiwemo spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula eneo hilo linapoweka mikakati ya mwelekeo wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Wetang’ula naye alihimiza umoja akisema eneo hilo litanufaika sana kwa kuzungumza kwa sauti moja katika masuala ya maendeleo ya kitaifa.

Baadaye katika mkutano wa mazishi katika kaunti ya Trans Nzoia, Mudavadi alihimiza wakenya waheshimu wadhifa wa Rais kama taasisi na ishara ya kuunganisha taifa.

Alisema Kenya itastawi na kufanikiwa wakati taasisi zinazotoa mwongozo zitaheshimiwa, kukuzwa na kulindwa huku akisisitiza haja ya nchi kusalia na umoja.

Mudavadi alihimiza wakenya wapuuze utamaduni wa propaganda ambao unasababisha migawanyiko, usambazaji wa taarifa zisizo sahihi na kufuta maendeleo ya uaminifu na ukweli.

Share This Article