Waziri wa Fedha John Mbadi, amelaani ghasia za kisiasa katika kaunti ya Homa Bay kufuatia kupigwa risasi na kuuawa kwa mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were.
Akizungumza katika hafla ya mazishi eneo la Suba Kusini, kaunti ya Homa Bay, Mbadi alitoa wito kwa asasi za uchunguzi kuharakisha na kuwakamata wahusika wa mauaji hayo.
Mbunge huyo alipigwa risasi na watu wasiojulikana siku ya Jumatano jioni karibu na mzunguko wa barabara ya makafani ya city, Jijini Nairobi.
“Nimehuzunishwa na kilichomkumba rafiki yangu ambaye nimefanya kazi naye bungeni kwa muda wa miaka saba. Nimezungumza na Rais na amekasirishwa sana na kisa hicho. Ameagiza wahusika wa mauaji hayo wakamatwe.
Mbadi alitaja kuwa ghasia za kisiasa zimeongezeka katika maeneo bunge ya Kasipul na Ndhiwa katika kaunti hiyo.
“Kuna ongezeko la ghasia katika kaunti ya Homa Bay na lazima tulaani ghasia hizo. Msiwauwe watu kwa sababu za kisiasa. Katika eneo la Ndhiwa watu wanashambuliana kwa kutumia mapanga kwa kisingizio cha kisiasa,” alisema Mbadi.
Waziri huyo aliwakosoa wanasiasa waaochochea ghasia, akisema wanahatarisha kutimuliwa kwa vyama vya kisiasa.
“Wale wanaochochea ghasia katika kaunti ya Homa Bay lazima wasitishe uovu huo. Huwezi walazimisha watu kukupigia kura,” alidokeza Mbadi.