Bustani za chakula kuimarisha utoshelevu wa chakula nyumbani na shuleni

Tom Mathinji
3 Min Read
Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh.

Utoshelevu wa chakula unasalia kuwa changamoto kuu Barani Afrika, huku mamilioni ya watu wakikabiliwa na baa la njaa na utapia mlo. Nchini Kenya takriban asilimia 30 ya familia zinakumbwa na ukosefu wa chakula cha kutosha hasaa katika maeneo kame , huku utapia mlo miongoni mwa watoto ukiwa katika viwango vya juu.

Kulingana na utafiti kuhusu Idadi ya watu na Afya (KDHS), asilimia 18 ya watoto walio chini ya umri wa miaka tano, wanakumbwa na changamoto ya ukuaji inavyostahili , asilimia 10 wana uzani mdogo na asilimia 3 wana uzani wa juu, hatua inayoleta taswira ya hali duni ya lishe hapa nchini.

Ili kukabiliana na swala hili, Mama Taifa Rachel Ruto kupitia mpango wake wa bustani za chakula nyumbani na shuleni almaarufu Mama Kitchen Garden, kwa  ushirikiano na wizara ya Kilimo na Ustawi wa Mifugo, anapigia debe kuimarisha utoshelevu wa chakula na kuboresha lishe shuleni na pia nyumbani.

Mpango huo unaangazia kilimo cha kuboresha lishe, utumizi wa teknolojia katika kilimo na kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia kilimo.

Aidha mpango huo unatoa changamoto kwa taasisi za elimu na familia kukumbatia bustani za chakula kama njia moja ya kuhakikisha upatikanaji wa vyakula vilivyo na rotuba sawia na kupigia debe elimu kuhusu kilimo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa ushirikiano kati ya sekta za kibinafsi na washirika wa mpango wa kitaifa wa bustani za chakula ulioandaliwa Jijini Nairobi, Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alisisitiza haja ya ushirikiano na mikakati jumuishi kufanikisha manufaa ya muda mrefu ya mpango huo.

Aliangazia umuhimu wa kuwa na bustani hizo za chakula shuleni, akisema zitawasaidia wanafunzi  kujifunza mswala kama vile  uchunguzi wa udongo, ukuaji wa mimea, kudhibiti wadudu na kilimo endelevu.

Katibu huyo alidokeza kuwa mpango huo utatoa fursa ya kuwaunganisha wanafunzi na wataalam wa kilimo kwa lengo la ubadilishanaji wa habari.

Elizabeth Koskei  Afisa Mkuu Mtendaji wa  Mama Doing Good.

Kwa upande wake Elizabeth Koskei  Afisa Mkuu Mtendaji wa  Mama Doing Good, shirika linalotekeleza mpango wa bustani za chakula kwa ushirikiano na wizara ya Kilimo, alisema mpango huo umejikita katika dhana kuwa wanawake, familia na jamii wana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao kwa kujitegemea kupata lishe bora.

“Lengo letu ni kwamba kila familia bila kuzingatia kiwango cha mapato au nafasi iliyopo, inaweza kuwa na bustani ya chakula itakayofanikisha upatikanaji wa vyakula na kufurahia afya njema kutokana na vyakula vilivyokuzwa nyumbani.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO) Dkt. Eliud Kireger na mwenzake wa kampuni ya Kenya Seed Sammy Chepsiror, pia walithibitisha kuwa wataunga mkono kikamilifu mpango huo kuhakikisha utoshelevu wa chakula kote nchini.

Uzinduzi rasmi wa bustani za chakula nyumbani utakuwa Mei 9, 2025 katika Taasisi ya Mafunzo ya Kilimo ya Koibatek, kaunti ya Baringo.

Share This Article