Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema kuwa serikali imejitolea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa maafisa wa usalama, kuhakikisha wanapata huduma bora za afya na malizo ya kumezewa mate.
Akizungumza leo Alhamisi alipowatembelea maafisa wa polisi wanaopokea matibabu katika hospitali moja Nairobi, Murkomen alisema maafisa hao wa usalama hujitolea mhanga kuhakikisha usalama unadumishwa nchini, na hivyo wanahitaji kupigwa jeki na serikali.
“Nilitumia siku kuu ya Labour Day kuwatembelea maafisa wa polisi wanaopokea matibabu katika hospitali ya Nairobi West, ambao walijeruhiwa wakiwa kazini,” alisema waziri huyo kupitia ukurasa wa X.
Kulingana na Murkomen, maafisa hao walipata majeraha wakikabiliana na uhalifu katika sehemu tofauti za nchi, akiwemo afisa mmoja kutoka nchini Haiti.
Katika ziara hiyo, Murkomen aliandamana na Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat na mwenzake Gilbert Masengeli, miongoni mwa maafisa wengine wakuu wa usalama.