Mbunge wa Kasipul Charles Were auawa Jijini Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read
Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were.

Mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa kwa pikipiki katika barabara ya Ngong Jijini Nairobi.

Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, gari la mbunge huyo aina ya Toyota Crown lilisimama katika taa za trafiki, kabla ya watu waliokuwa kwa pikipiki kulikaribia na mmoja wa abiria kwenye pikipiki hiyo kutoa bastola na kufyetulia gari hilo risasi.

“Abiria aliyekuwa kwenye pikipiki alikaribia gari hilo na kufyetua risasi kwenye gari la mbunge huyo, kabla ya kurejea katika pikipiki na kutoroka,” ilisema Huduma ya Taifa ya Polisi.

Licha ya kuwa kiini cha mauaji hayo hakijabainika, Huduma ya Taifa ya Polisi ilidokeza kuwa huenda mauaji hayo yalikuwa yamepangwa, na kwamba uchunguzi tayari umeanza.

“Maafisa Wakuu wa polisi walifika katika eneo la mkasa na uchunguzi umeanza kuhusu mauaji hayo,” ilisema Huduma ya Taifa ya Polisi Jumatano usiku.

Hapo awali mbunge huyo alikuwa amesema kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kufuatia visa vya ghasia vilivyoripotiwa katika eneo bunge lake.

Share This Article