Mwanamuziki wa mtindo wa dancehall nchini Uganda, Ziza Bafana, amemshtumu msanii wa muda mrefu Bebe Cool, kufuatia majigambo yake kwamba ana uwezo wa kushawishi nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya redio na televisheni kote nchini Uganda.
Hivi maajuzi Bebe Cool alijigamba kwamba anaweza kuamua ni nyimbo zipi zinapatiwa nafasi hewani, akitaja uhusiano wake wa karibu na wamiliki wa vituo vya habari.
Msanii huyo ambaye hujiita “bosi wa muziki” alisema uhusiano huo unampa uwezo wa kuendeleza au kuzima kazi za wasanii kwenye majukwaa mbalimbali.
Kauli hizo hazikupokelewa vizuri na wengi, hasa Ziza Bafana, ambaye alielezea matamshi ya Bebe Cool kuwa ya kuvunja moyo na yasiyofaa kuigwa hasa kwa sababu yametoka kwa mtu anayetambuliwa kama mwanzilishi na gwiji wa tasnia ya muziki nchini Uganda.
“Inasikitisha kusikia mambo kama haya kutoka kwa mtu ambaye anapaswa kuwa mfano wa kuigwa,” alisema Bafana akiongeza kusema kwamba udhibiti wa nyimbo zinazochezwa ili kupendelea wasanii fulani ni hatua inayozima vipaji na kuua ushindani wa haki.
Ziza Bafana alisisitiza kuwa wasanii chipukizi na wale huru wanategemea sana upatikanaji wa nafasi sawa kwenye vyombo vya habari ili kukuza taaluma zao.
Alionya kwamba tabia hiyo ya kudhibiti mambo inaweza kuzuia maendeleo ya tasnia nzima na kuunda mazingira yasiyofaa ambapo vipaji vinazimwa na ushawishi.
Madai ya Bebe Cool yamezua mjadala mkubwa katika tasnia ya muziki, huku mashabiki na wasanii wakisubiri kuona iwapo wasanii zaidi watakaojitokeza kuyalaani.