IG Kanja aagiza kuhamishwa kwa maafisa wakuu wa polisi Trans Mara

Tom Mathinji
1 Min Read
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, ameagiza kuhamishwa mara moja kwa maafisa wakuu wa polisi wanaohudumu katika eneo la Trans Mara, kaunti ya Narok kufuatia makabiliano yaliyoshuhudiwa katika eneo hilo na kusababisha vifo vya  waandamanaji watano.

Kanja, aliyezuru eneo hilo Jumanne akiwa ameandama na maafisa wakuu wa Huduma ya taifa ya Polisi,  alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI Amin Mohamed, kumhamisha afisa mkuu wa (DCI) katika eneo la Trans Mara kwa utepetevu wa kazi.

Inspekta Jenerali huyo aliwaambia wakazi wa eneo hilo kwamba uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na swala hilo, kubainisha chanzo cha ghasia hizo pamoja na kuwachukulia hatua wahusika.

Kulingana na Kanja, uchunguzi huo utatekelezwa na tume huru ya kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA), akidokeza kuwa  tayari maafisa wa IPOA wamewasili katika eneo hilo.

Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuwajibika kwa kudumisha amani na kuzingatia sheria.

Mnamo siku ya Jumatatu, ghasia zilizuka wakati wakazi walipowazuia masoroveya wa serikali kuingia kwenye ardhi ambayo inazozaniwa wakihofu kuwa wanapokonywa ardhi wanayodai wamerithi kutoka kwa wazazi wao.

Share This Article