Viongozi wa upinzani wameelezea wasiwasi kuhusiana na mchakato uliokamilika siku chache zilizopita wa kuwahoji wanaotaka kuhudumu kama Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Mahojiano ya kuwateua wote hao yaliendeshwa na jopo la uteuzi chini ya uenyekiti wa Dkt. Nelson Makanda.
“Tunafahamu kwamba jopo la uteuzi wa IEBC limehitimisha mahojiano na kwa sasa lipo katika mchakato wa kuhitimisha mchakato wa uteuzi. Tuna mashaka makuu kwamba hadi kufikia sasa, usimamizi wa mchakato wa uteuzi haujafikia viwango vya juu vya uchaguzi wa kuaminika,” walisema viongozi hao kwenye taarifa iliyotiwa saini na kinara wa PDP Martha Karua na Kalonzo Musyoka.
“Tunatumai katika awamu iliyosalia, jopo la uteuzi litaweka maslahi ya taifa mbele badala ya yale ya kibinafsi. Hata wakati huu wa lala salama, jopo la uteuzi linaweza likajiondolea lawama kwa kutoa ripoti ya kina ya utendakazi wao wakati likiondoka na kuwachagua Wakenya wanaosadikika kuhudumu kama Mwenyekiti na Makamishna wa IEBC,” iliongeza taarifa hiyo ambayo pia ilitiwa saini na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, Waziri wa zamani wa Utumishi wa Umma Justin Muturi na kinara wa DAP-K Eugene Wamalwa.

Viongozi wa upinzani wakishinikiza kuwa kabla ya uteuzi wa watakaohudumu kama Mwenyekiti na Makamishna wa IEBC, kutakuwa na mashauriano juu ya orodha ya mwisho kabla ya uteuzi wa mwisho kufanywa.
Jopo la uteuzi liliwahoji wagombea 11 wanaomezea mate uenyekiti wa IEBC huku wagombea wengine zaidi ya 100 wakihojiwa kwa nyadhifa za makamishna wa IEBC.
Katika mkutano wao wa leo Jumanne, Waziri wa zamani wa Usalama wa Taifa Dkt. Fred Matiang’i pia alihudhuria, ikiwa ni mara ya kwanza kwake kujitokeza hadharani tangu aanze kupendekezwa kugombea urais mwaka 2027.
Na huku viongozi hao wakianza kupanga mikakati ya uchaguzi mkuu wa 2027, haijulikani ni nani atakayegombea urais kati yao.