Peter Nwachukwu mume wa aliyekuwa mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili nchini Nigeria Osinachi amehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.
Jaji wa kike Njideka Nwosu-iheme wa mahakama kuu ya Abuja alitoa hukumu hiyo jana, miaka mitatu baada ya kifo cha Osinachi kilichotokea Aprili 8, 2022.
Katika uamuzi wake, jaji huyo alishikilia kwamba upande wa mashtaka ulidhibitisha makosa ya mshukiwa inavyohitajika kisheria na kuishia katika kumpata na hatia.
Nwachukwu alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 3, 2022 na afisi ya mwanasheria mkuu kwa niaba ya serikali ambapo alikabiliwa na mashtaka 23 likiwemo shtaka la mauaji ambalo adhabu yake inajumuisha kifo.
Makosa mengine ni pamoja na vitisho haramu, ukatili dhidi ya watoto na kupiga mkewe.
Kesi hiyo ilikuwa inafuatiliwa na wengi ndani na nje ya Nigeria kufuatia umaarufu wa mwendazake Osinachi.
Nwachukwu alikamatwa baada ya mwimbaji huyo kufariki akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja mjini Abuja ambapo awali aliaminika kuugua saratani ya koo.
Baadaye familia yake ilifichua kwamba Osinachi ambaye alikuwa na umri wa miaka 42 alikuwa anadhulumiwa na mume wake na dhuluma hizo ndizo zilimsababishia kifo.
Mashahidi 17 pamoja na watoto wake wawili, walifika mahakamani kutoa ushahidi wao baada ya kuitwa na upande wa mashtaka.
Marehemu Osinachi na mume wake Peter Nwachukwu wana watoto wanne.