Maafisa wa upelelezi wanaohusika na kesi zinazomkabili mwanamuziki P Diddy wamemlaumu kwa kile wanachokitaja kuwa mbinu za kuchelewesha kesi hizo.
Hii ni baada ya Diddy kupitia kwa mawakili wake kuomba jaji anayesikiliza kesi hiyo kuondoa ushahidi fulani huku tarehe ya kusikilizwa kwa kwesi hiyo ikikaribia.
Hata hivyo imebainika kwamba jaji tayari ametoa uamuzi kuhusu ombi la Diddy ambapo alisema waendesha mashtaka hawawezi kudhibitisha dai la kulazimishwa kufanya kazi kufuatia malalamishi ya mjakazi mmoja tu wa Diddy.
Lakini jaji huyo alikubalia waendesha mashtaka kutumia ushahidi kuhusu ulanguzi wa watu kwa ajili ya kuwatumia kingono ambao Diddy alikuwa anataka utupiliwe mbali.
Katika ombi lake kwa jaji, Diddy alidai kwamba waendesha mashtaka waliwasilisha ushahidi huo wakiwa wamechelewa na hivyo hakuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa kwa utetezi.
Maafisa wa upelelezi wanasema kwamba Diddy amekuwa akifahamu kwa miezi kadhaa kuhusu ushahidi ambao wanapanga kuwasilisha mahakamani na hatua yake ni ya kujaribu kumfanya jaji aahirishe kesi yake.
Hatua ya maafisa hao ya kuendelea kuleta ushahidi mpya imetajwa na mawakili wa Diddy kuwa kikwazo kwa uwezo wake kujiandaa kwa utetezi kwenye kesi hiyo inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Walipinga ombi la Diddy mbele ya jaji wakisema lililenga tu kupunguza uwezekano wa kudhibitisha makosa yake na hivyo kulazimu kesi kuahirishwa.