Shule nyingi kote nchini zitafunguliwa leo kwa ajili ya muhula wa pili wa mwaka 2025.
Huku hayo yakijiri, wasiwasi umetanda kati ya wazazi kuhusu kile kinachotajwa kuwa matozo ya shule yasiyo halali ambayo ni mzigo kwao.
Ripoti mpya ya kundi la Elimu Bora imefichua kwamba shule nyingi za umma zinatoza wazazi pesa ambazo hazijaidhinishwa rasmi.
Uchunguzi wa kundi hilo umeonyesha kwamba asilimia 90 ya shule za msingi na sekondari msingi zinaitisha wazazi ada ya kiingilio ya kati ya shilingi 500 hadi 25,000.
Wazazi wanalazimishwa pia kulipia vifaa mbalimbali kama madawati, makabati, vitabu vya kiada, masomo ya ziada na mitihani, gharama ambazo zinastahili kusimamiwa na pesa zinazotoka kwa serikali za kufadhili masomo.
Taarifa ya kundi la Elimu Bora inatoa mfano wa shule moja ya msingi katika kaunti ya Kisumu ambapo wazazi wanalipwa shilingi elfu 20 ada ya kiingilio.
Shule nyingine katika kaunti ya Mombasa inatoza wazazi shilingi 4,500 kwa kabati moja pekee huku kundi la Elimu Bora likionya kwamba ada hizo haramu zinafukuza wanafunzi shuleni.
Kundi hilo sasa linaitaka wizara ya elimu iingilie kati na kutatua suala hilo.