Meneja wa Spice Diana asifiwa kwa kujitolea kuhakikisha usalama wake

Roger anasemekana kuwekeza pakubwa katika kumpatia mwanamuziki huyo ulinzi wa hali ya juu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Marion Bosire
2 Min Read

Roger Lubega, meneja wa mwanamuziki Spice Diana, amesifiwa kwa kujitolea kwake katika kuhakikisha usalama wa Spice Diana na kuinua hadhi yake katika tasnia ya muziki.

Lubega, anayejulikana sana kama Manager Roger, anasemekana kuwekeza pakubwa katika kumpatia mwanamuziki huyo ulinzi wa hali ya juu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akizungumza katika mahojiano Ijumaa, Umar Bulega ambaye ni rais wa shirikisho la mabaunsa nchini Uganda alifafanua kuhusu sababu zilizosababisha ulinzi wa Diana uimarishwe.

Bulega alisema aliwasiliana na Manager Roger, ambaye alitaka kuhakikisha usalama wa Spice Diana kufuatia umaarufu wake unaokua kwa kasi.

“Karibu na mwanzo wa janga la COVID-19 mwaka 2020, Manager Roger alikuja kwangu akasema, alikuwa ameniona nikiwa na Jose Chameleone nikimlinda pamoja na timu yangu.” alisema Bulega.

Lubega alimwambia kwamba angetaka Spice Diana naye apatiwe ulinzi wa hali ya juu wa walinzi kama watano wenye viwango sawa na wale waliokuwa na Chameleone.

Wakati huo, janga hilo lilikuwa limesababisha kufungwa kwa sekta ya muziki.

Bulega alisema alijiuliza Roger angepata wapi fedha za kuendesha mpango mkubwa wa ulinzi kama huo. Hata hivyo, Roger alimhakikishia kuwa suala la kifedha halingekuwa tatizo katika mipango ya ulinzi.

Spice Diana mwenyewe alihusika katika kupanga mfumo wa ulinzi wake. Bulega alikumbuka kuwa aliwahi kuhamasishwa na wasanii wakubwa wa kimataifa waliokuwa wamezungukwa na walinzi wa hali ya juu.

“Aliniambia kuwa kuna baadhi ya wasanii wa kike duniani aliowapenda kwa jinsi walivyokuwa wanalindwa kitaalamu” alisema Bulega.

Alitaja wasanii kama Beyoncé na baadhi ya wasanii wa kike wa Tanzania waliokuwa wakifanya kazi na Diamond Platnumz. Alisema angetaka kuwa kama wao.

Bulega alisema uamuzi wa kuongeza ulinzi wake haukumletea tu Spice Diana ulinzi wa kiwango cha juu, bali pia uliimarisha hadhi yake ndani ya tasnia ya muziki.

Share This Article