Rais William Ruto jana aliungana na viongozi wengine ulimwenguni kuaga mwili wa Papa Francis katika uwanja wa St. Peter’s Square jijini Vatican.
Katika taarifa kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa X, Rais Ruto alisema kwamba ulimwengu umepoteza sauti ya huruma na yenye nguvu, iliyokuwa ikikumbusha wengi kwamba maendeleo muhimu na ya kweli hayaachi yeyote nyuma.
Kiongozi wa nchi aliendelea kusema kwamba papa Francis alionyesha ulimwengu kwamba namna bora ya kutumia uwezo ni kupitia huduma na kupitia utunzaji wa maskini na walio katika mazingira magumu watu wanaweza kuafikia mazuri ya kudumu.
Papa Francis alifariki Jumatatu ya Pasaka baada ya kukumbwa na kiharusi na matatizo ya moyo na alizikwa jana katika hafla iliyohudhuriwa na waumini wengi.
Miongoni mwa viongozi waliokuwepo ni Rais wa Marekani Donald Trump, Javier Milei wa Argentina, waziri mkuu wa Italia Georgia Meloni na Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr.
Mwili wa Papa Francis ulizikwa kwenye kanisa la St. Mary Major huko Roma, ambako alipenda kwenda sana kwa ajili ya maombi wakati akihudumu kama Papa.
Francis ndiye Papa wa kwanza amezikwa katika kanisa hilo la Santa Maria Maggiore Basilica baada ya miaka 350 wakati Papa Clement wa 9 alizikwa humo.
Waumini wanaweza kuzuru kaburi la Papa Francis kuanzia leo asubuhi kulingana na tangazo la Vatican.