Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa anayejihusisha na uuzaji na ununuzi wa simu zilizoibwa katika kaunti ndogo ya Naivasha, kaunti ya Nakuru.
Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, walimkamata Peter Mburu mwenye umri wa miaka 33, baada ya kufanya msako kwenye duka lake Naivasha mjini.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema kuwa mshukiwa alipatikana akiwa na simu kadhaa zinazoshukiwa kuwa za wizi.
Aidha, maafisa hao pia walipata tarakilishi moja na vifaa vingine ambavyo hutumiwa kuondoa alama za siri za rununu hizo.
Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Naivasha, akisubiri kufikishwa mahakamani.