Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo Alhamisi Aprili 24, 2025, kujibu shtaka la uhaini ambalo adhabu yake ni kifo, wiki chache baada ya chama chake kufungiwa kushiriki uchaguzi ujao.
Mamlaka nchini humo zimekuwa zikikandamiza chama cha upinzani Chadema kwa kiasi kikubwa nchi hiyo inapoelekea uchaguzi wa urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.
Chadema kinamtuhumu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejelea mbinu za ukandamizaji zilizotumika na mtangulizi wake, John Magufuli.
Shirika la Amnesty International limeitaka serikali kumuachilia Lissu mara moja bila masharti yoyote, huku naibu wake, John Heche, ambaye pia alikamatwa kwa muda mfupi wiki hii, akihimiza maandamano.
Lissu, wa umri wa miaka 57, alitarajiwa kufikishwa mahakamani katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam leo asubuhi.
Hajaonekana hadharani tangu alipofikishwa mahakamani kwa muda mfupi Aprili 10, aliposomewa mashtaka ya uhaini — shtaka lisilo na dhamana — pamoja na kuchapisha taarifa za uongo.
Wakati huo, Lissu aliambia umati wa wafuasi wake kwamba kesi ya uhaini ni njia ya ukombozi.
Amewahi kukamatwa mara kadhaa awali, lakini hii ni mara ya kwanza anakabiliwa na shtaka kubwa kama hilo.
Kiongozi huyo mwenye msimamo mkali ameongoza upinzani mkali dhidi ya serikali, akiahidi kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi bila marekebisho makubwa kutekelezwa kwenye mfumo wa uchaguzi.
Hatua ya CHADEMA ya Kukataa kutia saini kanuni za mwenendo wa uchaguzi ilisababisha kifungiwe nje ya uchaguzi, lakini chama hicho kimesema kanuni hizo zilitungwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba chama tawala kinaendelea kubakia madarakani na kwamba kuenguliwa kwake hakukuwa kwa mujibu wa katiba.
Matumaini yaliyozimwa
Chama cha rais, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilishinda kwa kiwango kikubwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, lakini Chadema inasema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwani wagombea wake wengi waliondolewa kiholela.
Chadema kimekuwa kikidai marekebisho ya uchaguzi, yakiwemo kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na kuweka kanuni wazi za kuhakikisha wagombea hawatolewi kiholela kwenye kinyang’anyiro.
Lissu alionya mwaka jana kuwa Chadema kitazuia uchaguzi kwa njia ya mapambano iwapo mfumo hautarekebishwa.
Matakwa ya upinzani yamepuuzwa kwa muda mrefu na chama tawala.
Lissu, ambaye ni wakili kitaaluma, alijiunga na Bunge mwaka 2010 na kugombea urais mwaka 2020.
Alipigwa risasi mara 16 katika shambulio la mwaka 2017 ambalo anaamini liliagizwa na wapinzani wake wa kisiasa.
Baada ya kushindwa uchaguzi wa 2020 dhidi ya Magufuli, alikwenda uhamishoni akarejea mwaka 2023 akiwa na matumaini mapya kufuatia hatua za Rais Hassan kulegeza baadhi ya vikwazo vya utawala wa awali dhidi ya upinzani na vyombo vya habari.
Hata hivyo, matumaini hayo hayakudumu, huku mashirika ya haki za binadamu na serikali za Magharibi zikiikosoa vikali serikali kwa kurejea katika ukandamizaji, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa wanasiasa wa Chadema pamoja na visa vya utekaji na mauaji ya wanasiasa wa upinzani.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kukamatwa kwa Lissu, Amnesty ilieleza kuwepo kwa “kampeni ya ukandamizaji” kutoka kwa mamlaka, ikikosoa mbinu “za nguvu kupita kiasi kuwakandamiza wakosoaji.”