Liverpool wanusia ubingwa baada ya Arsenal kubanwa na Palace

Liverpool huenda wakatawazwa mabingwa Jumapili hii watakapowaalika Tottenham Hotspur, endapo watapata ushindi au kutoka sare.

Dismas Otuke
1 Min Read

Liverpool wanahitaji alama moja pekee katika mechi tano zilizosalia  kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu Uingereza (EPL) msimu wa mwaka 2024-2025.

Wekundu wa Anfield Liverpool, walinusia ubingwa jana usiku bila kugusa mpira, baada ya wapinzani wa karibu Arsenal, kupoteza uongozi mara mbili na kutoka sare ya 2-2, nyumbani dhidi ya Crystal Palace.

Yakub Kiwior, na Leandro Trossard, walipachika mabao ya wenyeji the Gunners kunako kipindi cha kwanza, huku Eberechi Eze, na nguvu mpya Jean Phillipe Mateta, wakipachika magoli ya Palace, moja katika kila kipindi.

Sare hiyo ilikuwa ya 13 kwa washika bunduki hao wa London msimu huu, wakiwa na alama 67, pointi 12 nyuma ya Liverpool walio na mechi moja mkobani.

Liverpool huenda wakatawazwa mabingwa Jumapili hii watakapowaalika Tottenham Hotspur, endapo watapata ushindi au kutoka sare.

The Reds wamenyakua ubingwa wa Ligi kuu EPL mara 19 wakiwania taji ya 20, na la kwanza tangu msimu wa mwaka 2019 na 2020, wakiwa chini ya uongozi wa kocha Jurgen Klopp.

Share This Article